MISTARI YA WIMBO HUU

Naamka asubuhi nipo chwiri tena mapema
Nautoa mkeka sakafuni kisha nauhukunja vyema
Nawaza nitakula nini mentali kisha naguna
Naanza kujikongoja kichwa chini mikono nyuma
Naelekea kilingeni nilikopaki mkokoteni
Nasaga na rumba kimshazali nyie acheni
Nawapa ‘Hi’ machizi wananipa peace tunafurahi
Tunapiga stori nyingi walah bila maslah
Mara napata zali napeleka kago uswahili
Wananipa bukumbili dangaa chee nazisunda chini
Wakati natoka huku kijasho chembamba kikinitoka
Nikaona toto ya nguvu nikajikuta nimeropoka
“Dada habari samahani naomba niulize swali”
Akajibu “maskini koma tafadhali hii ngoma ya gari”
“Ehee unajua dada”, “we vipi hebu nipishe”
“Dada mbona mkali”, “wee kinyago kubali yaishe”
Nikasema Inshala sawa hiyo yote kwa sababu ya fukara
Nisije nikakubaka nitupwe selo nikawe kafara
Nikaachana nae sehemu za nyuma akizitingsha
Nilikula kwa macho hali yangu haikuridhisha
Nageuza mkokoteni nakuelekea maskani
Nikawapa stori machizi wakanicheka ikawa utani
Siku moja nililemaa maskani sikuwa na tenda
Na nilikuwa nikitafakari ni vipi siku itakwenda
Kumbe kuna gari ilikuja na kupaki karibu yangu
Sikuweza kuisikia labda sababu ya njaa yangu
Nilishtushwa ghafla na mlio mkali wa honi
Nilipatwa na mshtuko na hofu kubwa moyoni
Kuangalia pembeni ilikuwa imepaki Toyota Surf
Kulikuwa na sura ngeni ya malaika akaomba tafu
Nilisita kunyanyuka kwa sababu nilikuwa mchafu
Na alitoa elfu kumi na alikuwa akitaka dafu
Nilipokea hela alichotaka nilimletea akakipokea
Tabasamu zito akanitolea nilimpa chenji
“Ohh no keep chenji una mawazo mengi itakufariji week end”
Alikunywa maji ya dafu alitupa na kunikonyeza
Niliganda kama nyamafu nikahisi alinibeza
Alinipa busu la huba shavuni akanichombeza
“I love You” akawasha gari akateleza

Zali la mentali
Limetokea wakati mimi nna njaa
Nikapendwa na demu mkali
Na kuwaacha watu wote wakinishangaa
Katika mitaaa

Zilipita siku mbili nikiwaza kilichotokea
Nikawaza yule ni mtu au jini amenitokea
Potelea mbali uchawi hauendi kwa mentali
Narudi nanyonya napuliza mentali nakuwa shwari
Nabeba rumbesa nakatiza Samora Avenue
Mara kwa ghafla mbele yangu inapaki Toyota mark II
Ohh napata ghadhabu mara nyingi sipendi dharau
Naifuata gari kuanza kupaka mara nahema juu juu
Aah ni yule mrembo!
“Maskini pole sana mzigo mbona mzito kweli utafika nao salama”
Natabasamu “Oh nimeshazoea mama
Na namshukuru Mwenyezi Mungu kwani hii ni kama karama”
Anakuwa mnyonge anakata kucha anantazama
Anaaza kulia anatoa leso anainama
“Namwambia bibie ni mara ya pili tunaonana
Na sidhani kama ni mbaya iwapo tutafahamiana”
“Naitwa Vick nina miaka 22
Ni mtoto wa kipekee kwenye familia ya kitajiri”
“Oh naitwa Jay ukiniita fukara haukosei
Na naishi kwa nguvu za macho siku zenyewe hazisogei”
Alishuka toka garini na kusema “Jay nakupenda”
Akaruka kwangu mdomoni nakuanza kupata denda
Nilichomoka kwake na kuanza kurudi nyuma
“Tafadhali mpenzi Jay jamani nionee huruma
Acha kubeba mizigo panda ndani kwenye mchuna
Twende Mbezi Beach kwangu upepo unapovuma”
Sikiliza Vick napenda tuwe marafiki
Lakini hadhi yako hutakiwi kuwa na mtu wa dhiki
Hata wazazi wako naaamini hawataafiki
Tajiri na tajiri maskini thithaminiki
Tafuta kibopa mwenzio ili usishushe hadhi yako
Mimi sistahili hata kuwa kijakazi wako
“Tafadhali Jay usitamke maneno hayo
Naomba unielewe haya machache niyasemayo
Hadi huu wakati mimi nimekupenda kwa dhati
Ukikubali niwe wako nitajiita mwenye bahati”
Nimeelewa Vick naomba niwahishe mzigo
Tajiri ni mkorofi anan’subiri migomigo
Na kila nikichelewa mwenzako napata kipigo
Nasaga na rumba jua na mvua kwa mpigo
Tuliongea mengi akanipa hela za matumizi
Sikuwahi hata kuziona nilikuwa kama chizi
Niliacha kubeba mizigo penzi letu likaota mizizi
Watu wa uswahili wakasema natumia kizizi

Zali la mentali
Limetokea wakati mimi nna njaa
Nikapendwa na demu mkali
Na kuwaacha watu wote wakinishangaa
Katika mitaaa

Baada ya miezi mitano Vick alipata ujauzito
Tulifurahi sana mambo yakawa mpwito-mpwito
Swala la kwenda kwa wazazi wake halikuwa zito
Walifurahi sana kuniona tukafanya tambiko
Walisema Jay maisha ya Vick yapo chini yako
Tumefurahi mmpendana kumlea ni jukumu lako
Ilipangwa mikakati kamambe ya kufunga ndoa
Watu hawakuamini kama mimi vipi nitamuoa
Ilifika siku ya siku mentali Jay ndani ya jumba
Na Vick ndani ya shela hakuna uchawi wala ndumba
Tulishikana mikono ni nderemo na vifijo
Tukafunga pingu za maisha kanisani bila ya fujo
Furaha isiyo kifani lilifanyika bonge la party
Watoto wa uswahili walibeba wali kwenye mashati (duh!)
Zawadi zilizagaa zilikuwa nyingi tena kemkem
Baba mkwe alitupa benzi, kiwanda nyumba na bm
Acha zawadi nyingi kutoka kila sehemu
Nilikumbuka nikacheka nilivyoteswa na wale mademu
Mambo swadakta nipo na Vick ndio my wife
Kidume nang’aa wanajigonga shenzi type (shenzi type)
Nilipokuwa arosto mlinikwepa kama ukoma
Mambo juu ya mstari kunisalimu mnaona noma
Sasa hivi napeta nabadili gari full kipupwe
Mlio nicheka wanataka ardhi ipasuke
Naelekea kilingeni kuwapa dili machizi wangu
Tena mara kwa mara siwezi kuwacha asili yangu
Vick ni Jay, Jay ni Vick mustarehe kutoka ndani ya dhiki
Sasa kila siku sherehe ahaaaa!

Zali la mentali
Limetokea wakati mimi nna njaa
Nikapendwa na demu mkali
Na kuwaacha watu wote wakinishangaa
Katika mitaaa

Toa Maoni Hapa

SHIRIKISHA MWINGINE

Your email address will not be published. Required fields are marked *

SHIRIKI KUONGEZA MISTARI