Picha kwa hisani ya Mtandao wa Bongo5

NAPATA ukakasi ninaposikia matangazo ya muziki wa taarabu au bendi inayopiga taarabu, kwani ninapoingia kwenye kumbi unapopigwa muziki huo, sisikii taarabu hata moja.

Kwa mtizamo wangu na kwa jinsi ninavyoifahamu taarabu, hiki kinachopigwa sasa na kuitwa taarabu sicho. Ni udanganyifu mkubwa.

Labda kwa kuwa wanamuziki na viongozi wao wameweka kionjo ili waweze kupoteza maana ya taarabu kwa kuiita Modern.

Kwenye taarabu hakuna Modern na ndiyo maana wanaofahamu maana hasa ya muziki huu, wanauita asilia kwa kuwa uliopo sasa ni wa sasa lakini unachanganywa na taarabu.

Taarabu asili yake ni ustaarabu, utaratibu, upole na uungwana. Zaidi ya yote ni muziki wa kutoa burudani na kusikilizwa na yeyote bila kuwa na hofu ya mashairi.

Hivyo hii tunayoisikia sasa siyo taarabu bali ni aina fulani ya muziki ambao sitakosea nikiuita kuwa ni muziki wa ‘Rusha roho’, ‘Kiduku’, ‘Mnanda’, ‘Mipasho’ au aina nyingine na siyo taarabu ninayoifahamu.

  • Taarabu ni muziki wa asili ya Pwani ya Afrika Mashariki na una mchanganyiko na ala za muziki wa Afrika ya Kati na India kwa kuwa wanatumia filimbi na Kaswida za Kiislamu.
  • Tangu enzi, taarabu ilikuwepo na uchezaji wa aina yake ambapo ni moja ya burudani isiyovunja utamaduni wa Mwafrika.
  • Ni muziki wa kiistaarabu na wenye mashairi ya kiistaarabu na unapingana kwa kiasi kikubwa na huu wa sasa wenye vikumbo na ugomvi wa maneno yasiyokwisha.
  • Asili ya muziki hii siyo kucheza bali kutazama na kutunza na kwa kusikiliza na kuangalia. Ni tofauti na taarabu ya sasa yenye mrengo wa tunzi za matusi, malumbano, umwamba na hauna usiri wala tafsida.
  • Sifa ya taarabu asilia inabaki pale pale, kwani haukuwa tu ni burudani bali pia ulifundisha kwa kubembeleza na kuasa.

Muziki huu haukuwa na matamanio ya kuonyesha umwamba kati ya wasanii, nani bingwa wa mapenzi, nani mshindi wa kuandika mashairi yenye ukakasi na maadili.

Muziki huo unaendelea kuwa kwenye heshima yake na anayeupiga ni lazima aupige kwenye midundo hiyohiyo bila kubadilisha kama ilivyokuwa kwa muziki wa ‘Country’.

Muziki wa Country uliopigwa miaka mingi iliyopita, hauna tofauti na ule unaopigwa miaka ya sasa.

Midundo yake inabaki kama ilivyo, na kama kuna mabadiliko, basi siyo ya kuuvuruga wote kama tunavyoshuhudia kwenye taarabu miaka ya sasa.

Mwanamuziki mkongwe wa taarabu nchini, Hadija Omari Kopa ambaye amefikia kuitwa Malkia wa mipasho, hivi karibuni Mwananchi ilimkariri akisema kuwa muziki wa taarabu asilia utaendelea kuwepo.

Anakwenda kinyume na kile kinachoitwa Modern Taarabu na kusema, aina hii ya taarabu ni suala la muda tu kwani unapita.

Namnukuu: “Taarabu asilia ulikuwa ni muziki wa kuvutia na utaendelea kuwa hivyo siku zote. Muziki wa Modern Taarabu hauwezi kuvutia wala kudumu.”

Baadhi ya waimbaji wakongwe wa muziki wa taarabu asilia ni Fatuma Binti Baraka, ‘Bi Kidude’, Juma Bhalo, marehemu Issa Matona Patricia Hillari na wengine wengi.

Kwa mifano hiyo na mingine mingi, naweza kusema taarabu asilia ni muziki wetu na ni sifa ya taifa kwa kuwa nchi yetu ni moja ya nchi zilizopo Ukanda wa Afrika Mashariki.

Ndiyo nasema ina hadhi na sifa yake kwa kuwa hakuna aliyewahi au kujaribu kuubadilisha muziki huu na hakuna atakayepata fursa ya kufanya hivyo kwani sifa yake ni kuwa vile ulivyo.

Muziki wa taarabu una mambo ambayo kamwe hayawezi kufananishwa na taarabu ya midundo ya modern.

Nachokiona mimi hapa, wasanii wanajaribu kuchanganya mambo ili kupata soko la muziki litakaloweza kuufunika muziki asili wa taarabu.

Hivyo basi kuna kila sababu ya kuhakikisha muziki huu heshima yake inaendelea kuwapo kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho.

Kwa siku za karibuni naona muziki huu umekosa mwelekeo na kukosa heshima yake ya kawaida kama ilivyokuwa hapo zamani.
Naamini wadau wa burudani wakishirikiana na Serikali kupitia wizara husika, kila kitu kitakuwa sawa na kulinda hiki kielelezo cha Utamaduni wa Mwafrika.

Tuulinde na kuuenzi muziki huu na zifanyike jitihada za kuwakwepa wale wote wanaojaribu kuutoa kwenye mstari wake wa kweli kiasilia.

Kukaa kimya na kuacha sanaa hii ya muziki ikipotea njia, yaani ikiupoteza muziki wa taarabu halisi na kuupeleka kwenye taarabu ya kisasa iliyokosa mafunzo, zaidi ya vijembe na malumbano, tutakiathiri kizazi kijacho.

Jukumu hili linapaswa kuwa ‘msalaba’ wa wote, kila mwenye kuguswa na jinsi mambo yasivyokwenda vizuri kwenye muziki wa taarabu, basi abebe jukumu la kurekebisha.

Makala hii ilichapishwa kwenye Gazeti la Mwananchi tarehe 22 Februari 2013.

Toa Maoni Hapa

Added by

daniel

SHARE

Your email address will not be published. Required fields are marked *