NAOMBA nianze makala ya leo moja kwa moja kwa kuuliza swali. Wimbo ni mali ya nani miongoni mwa wanamuziki wa Tanzania?

Sababu ya kuuliza swali hili ni migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza miongoni mwa wanamuziki wetu kudaiana uhalali wa umiliki wa nyimbo.

Naomba nitoe mifano miwili ya matukio ya hivi karibuni. Mfano wa kwanza ni mgogoro baina ya Hafsa Kazinja na Banana Zorro wa uhalali wa matumizi kibiashara ya wimbo “Pressure” wa Bi Hafsa aliomshirikisha Banana Zorro.

Mfano wa pili ni wa wimbo “Salaam Kwa Mjomba” unaojulikana kuwa ni wa Irene Sanga ambaye alimshirikisha Mrisho Mpoto.

Migogoro ya nyimbo hizo kwa wasanii hao inafanana. Nayo ni kwamba walioshirikishwa wanadaiwa kuzitumia kibiashara kazi za waliowashirikisha bila idhini ya wenye kazi hizo.

Kinachosemekana ni kwamba Banana kwa upande mmoja na Mpoto kwa upande mwingine wanaweza kupata mialiko ya kibiashara na kuzitumia kazi hizo, kila mmoja kwa aliyoshiriki, kutumbuiza kwa kusaidiwa na kanda (kwa “playbacks”) pekee au na waigizaji wa Hafsa kwa Banana na Sanga kwa Mpoto.

Hilo ndilo linalodaiwa kumkera Hafsa kwa upande wake na Sanga kwa upande wake pia.

Inaaminika Banana na Mpoto wako katika nafasi nzuri ya kupata “dili” hizo kwa sababu ya umaarufu wao uliowazidi waliowashirikisha na kwa sababu pia ya ushiriki wao mkubwa zaidi kwenye nyimbo hizo unaolingana au hata kuzidi ule wa waliowaalika.

Banana alianza kufahamika siku nyingi tangu akiwa mdogo kupitia kundi la ke na kijana mwenzake Masiga la B Love M walipoinuliwa na wimbo wao wa “Anakudanganya”, wakati Hafsa ana miaka michache tangu afahamike.

Kwa upande mwingine, Mpoto alianza kujulikana tangu alipoigiza kama muuza duka katika tangazo lililokuwa likionyesha hujuma ya manunuzi ya bidhaa za shule.

Vile vile, alipata umaarufu pia katika tangazo la biashara la dawa ya kuuwa mbu ya kufuliwa kwenye chandarua.

Irene amejulikana hivi karibuni kupitia tungo zake zilizokwenda shule ukiwemo huo wenye mgogoro, tungo zilizonifanya nimpende kuzidi maelezo! Sasa linapojitokeza suala la mialiko ya kutumbuiza, watu huwaangalia zaidi Mpoto na Banana.

Pamoja na kupinga kwangu matumizi yoyote ya kazi za sanaa ambazo msanii hana uhalali nazo kuzitumia kibiashara lakini siamini kama dada Sanga aliifanya kazi ya wimbo wa “Salaam kwa Mjomba” bila mchango hata mdogo wa Mpoto.

Siamini kama mashairi yale yote ya wimbo huo yalitungwa naye bila Mpoto kuchangia chochote. Aidha, siamini kama Hafsa alitunga kila kitu katika wimbo wa “Pressure” bila Banana kuongeza chochote.

Siamini kabisa kwamba hata ule mstari ambao Banana ameimba kwa sauti ya marehemu Moreno wa bendi ya Moja One ya Kenya unaoimbwa “kama zamani na sasa kuna tofauti, tumalizee tofauti zetu e mimi na wewe e tofauti zetu e” haukuwa ubunifu wa Banana mwenyewe.

Kama mstari huo haukua ubunifu wake lakini lazima kuna vitu amechangia katika kuuboresha wimbo huo.

Ukweli kwamba wasanii wanaposhirikiana kwenye wimbo husaidiana kuuboresha unaonekana wazi katika wimbo wa Nguza Viking wa “Tafadhali” aliomshirikisha Solo Thang.

Kwa asili yake, wimbo huo ulirekodiwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na Marquz Original mwaka 1984 wakati huo bendi hiyo ikitumia mtindo wa Zembwela. Ulirekodiwa pamoja na nyimbo za “Sofia Namba moja”, “Wakati Nilikuwa Mdogo”, “Mpenzi Lutta”, “Sumu ya Mapenzi”, “Karubandika” na “Ni wewe pekee”.

Wimbo ule wa asili haukuwa na mashairi yoyote ya kughani na huu wa mara ya pili una mashairi hayo yaliyoghaniwa na Solo Thang.

Mashairi hayo ya kughani, moja kwa moja yalikuwa kazi ya Solo Thang. Siamni kama Nguza aliyatengeneza yeye, kwa sababu ni sehemu ya sanaa asiyo na utaalam nayo.

Tumia mtazamo huu huu kwa kuangalia tunzi kama za “Crazy Over You” wa Klynn aliyemshirikisha “Mgumu” Chid Benz katika kufokafoka na nyimbo zote wanazoshirikiana wanamuziki wanaoimba na wanaoghani (wanaorap).

Ni wazi kazi ya kughani inaandaliwa na hao hao wanaoghani. Ndiyo maana haikushangaza baadhi ya vituo vya redio kuutaja wimbo wa “Tafadhali” kuwa wa Solo Thang aliyemshirikisha Nguza Viking, jambo ambalo Nguza alilisahihisha kupitia vyombo vya habari.

Katika hali kama hiyo, mtu anapotoa mchango mkubwa katika utunzi wa wimbo, nini kitamzuia asijione naye ana haki katika matumizi ya wimbo huo ingawa anajua wazi si wake?

Nilianza makala haya kwa kuuliza swali la wimbo ni mali ya nani miongoni mwa wanamuziki wa nchi yetu. Miaka kadhaa nyuma, kama mpenzi wa muziki na sanaa (si mdau kwani kupenda tu kitu hakumfanyi mpenda kitu huyo kuwa mdau wa kile kitu) nilifanya utafiti wa kujua wimbo wa bendi ya muziki ni mali ya nani.

Kilichonisukuma nifanye utafiti huo ambao ungechapishwa kwenye moja ya magazeti ya Kiswahili yaliyokuwepo wakati ule ni tabia iliyozuka wakati huo na kupamba moto sana ya wanamuziki mbalimbali kuzuia matumizi ya nyimbo walizotunga na bendi walizohama ili wakazitumie walikohamia.

Hebu angalia orodha hii:- Cosmas Chidumule aliondoka kutoka Kurugenzi ya Arusha na nyimbo “Neema” na “Majirani Huzima Redio” na kuzirekodi na DDC Mlimani Park mwaka 1985 mwishoni.

Kurugenzi nao, chini ya mkongwe Lazaro Bonzo, waliurekodi wimbo wa “Majirani Huzima Redio” kwani alipohama bendi, Chidumule hakuizuia Kurugenzi kurekodi wimbo huo.

Ramadhani Kinguti, “Kinguti System” naye mwaka 1988 aliondoka na wimbo wa “Wenye Nyumba Msiwaudhi Wapangaji” uliokwisharekodiwa RTD na DDC Mlimani Park na kuurekodi tena akiwa na Bicco Stars.

Sikinde waliurekodi wimbo huo wakati Kinguti alishahama na hivyo kumfanya Benno Villa aimbe sauti tofauti katika wimbo huo ikiwemo yake na ya Kinguti katika vipande tofauti.

Shaaban Dede naye alipotoka Bima Lee mwaka 1987 mwishoni na kujiunga tena na Msondo, Bima walilalamika aliondoka na wimbo wao “Sauda”. Kipande kidogo cha wimbo huo kiko hivi: “Siku tutafunga ndoa ee shangwe, hata ndege wataimba kwa furaha.

TX Moshi William aliimba katika wimbo huo: Sauda washa taa unitoe gizani, ndugu na marafiki wafurahi, mahasidii washikwe na mshangao…

Dede: Kama kweli wanipeenda fika kwa wazazi wangu, isiwe lengo lako ni kuniharibia maisha, nikabaki kuzurura mshahara kuchoka na jasho kuniitoka, mavumbi telee”.

Orchestre Safari Sound ya Mtindo wa Power Iranda nayo ilichangia wimbo wa “Kulala Sebuleni” na Washirika Tanzania Stars “Watunjatanjata” mwaka 1990 ambapo Kamanda Muhidin Maalim Gurumo anasemekana kutoka na wimbo wa “Wosia kwa Watoto” kutoka OSS mwaka 1991, akapita nao Sikinde na kutua nao Msondo alikorekodi nao mwaka huo huo 1991. Orodha ni ndefu lakini kwa leo itoshe hapo.

Hiyo ndiyo hali iliyonipa changamoto kufanya utafiti huo ambapo kwa ujumla wake nilipata aina zifuatazo za majibu.

Kwanza, wimbo ni mali ya mtunzi kwa sababu akili yake ndiyo iliyobuni kilichotungiwa wimbo. Kwa hiyo ni mali yake isiyopaswa kwa namna yoyote kuondolewa kwenye umiliki wake.

Pili, wimbo ni mali ya bendi kwa sababu mpaka ukamilike wanamuziki mbalimbali katika bendi hutoa mchango wa kuufanya ukamilike kutegemeana na vyombo wanavyopiga.

Aina ya tatu ya jibu nililopata ni kwamba wimbo ni mali ya mtunzi kama kweli yeye ni mtunzi. Nilitajiwa wakati huo watunzi wachache wa kweli wa Tanzania kuwa Jabali Marijan Rajab, Remmy Ongala, Cosmas Chidumule, TX Moshi William, Benno Villa Anthony na Max Bushoke.

Wengine nilitajiwa kuwa Joseph Mulenga, Hamza Kalala, Eddy Sheggy, Jerry Nashon, John Kitime na Suleiman Mwanyiro.

Nilielezwa kwamba wanamuziki hao ambao baadhi ni marehemu na wengine niliowasahau wanatengeneza wazo, wanaliwekea kiimbo(tune), wanawaelekeza wenzao jinsi ya kuimba na wanaelekeza upigaji wa vyombo kwa asilimia kubwa ya vyombo, hasa vya magitaa.

Hao hutengeneza hasa muziki na si kupeleka wazo tu la wimbo. Kwa hiyo wanamuziki wa aina hiyo wana haki kudai kuwa nyimbo wanazotunga ni mali yao ingawa hata wao, baadhi hawakutunga kwa asilimia mia zote.

Katika jibu hilo, niliambiwa niwajumuishe King Michael Enock “Teacher” na Joseph Lusungu ambao kwa sasa wote ni marehemu ambao hawakusikika kama watunzi sana hasa King Michael lakini walikuwa wataalam wa hali ya juu wa kutengeneza nyimbo kwa kuzipanga vizuri baada ya kukamilishwa kutungwa.

Niliulizwa kutokana na mchango wao mkubwa wa kuziboresha nyimbo, kulikuwa na uhalali gani watunzi wa bendi zao za Msondo kwa Lusungu na Sikinde kwa King Michael wazidai nyimbo hizo kuwa zao walipohama bendi?

Nne, nilielezwa kuwa nyimbo zote za bendi ni mali ya mwenye bendi yeyote yule, mtu binafsi, taasisi, chama, wanamuziki wenyewe na kadhalika kwa sababu utunzi wa nyimbo hizo umefanywa ndani ya mkataba wa ajira, kwa malipo ya mshahara kwa mtunzi na kwa kutumia vyombo vya muziki vya mwajiri.

Lipi ni sahihi zaidi katika majibu hayo si kazi yangu kuamua kwani yote yana hoja za kushawishi lakini kuna mtunzi mmoja mahiri sana wa wakati huo alitoa kauli iliyonisisimua sana wakati nikikusanya hoja hizo.

Alisema mtu anayelazimisha kuhama bendi na nyimbo alizotunga na bendi hiyo ni mtunzi wa kubahatisha. Alifafanua kwamba mtunzi makini asiye wa kubahatisha siku zote huangalia mbele. Alizokwishatunga zimepita, anafikiria kutunga nyingine aendako.

Ukitafakari hoja hii unaweza kukubaliana na mwanamuziki huyo kwa kuangalia jinsi marehemu TX Moshi William alivyoachana kabisa na tungo zake nyingi na nzuri alizotunga akiwa na Polisi Jazz Band, Wana Vangavanga mara alipohamia Msondo.

Hakushughulika kabisa na nyimbo hizo kwa miaka yote 24 aliyodumu na Msondo Ngoma.Vilevle, wakati Sikinde inarekodi nyimbo mpya RTD mwanzoni mwa mwaka 1983 zikiwemo nyimbo zake mbili, Max Bushoke hakuwa na bendi hiyo lakini hakuzuia kurekodiwa kwa nyimbo hizo “Kupenda Siyo Ndoto” na “Utamaduni” zilizoimbwa kwa umahiri mkubwa na Hassan Rehani Bitchuka.

Nyingine walizorekodi Sikinde mwaka huo na watunzi wake kwenye mabano ni “Nelson Mandela” (Joseph Mulenga), “Usitumie Pesa Kama Fimbo” na “Tumetoka Mbali” (Cosmas Chidumule), “Usinichukie Bure” (Muharami Saidi) na “Watoto Wanakimbia Nini”(Shaaban Dede).

Kwa miaka hii ya karibuni, wimbo ulio utunzi wa Benno Villa unaobeba jina la albamu ya Sikinde ya “Huruma kwa Wagonjwa” ulitungwa mwanzo na Hussein Jumbe kama “Nani Kaiona Kesho” aliokwenda kuutumia TOT Band.

Lakini baadaye alirudi Sikinde na kukutana tena na “Huruma Kwa Wagonjwa”! Sasa Hussein Jumbe huyo yuko Mikumi Sound ya Morogoro ambapo Sikinde wameshaweka wazi kwamba kwenye albamu yao ijayo hawatajumuisha wimbo mzuri sana utunzi wake uitwao “Hamnazo”.

Hapo ndipo ninapouliza tena kama wimbo huo si mali ya Sikinde walioutengeneza na kuuboresha.

Wakati nikisubiri majibu ya wadau na wapenzi wa muziki ya swali la muziki ni mali ya nani kupitia namba yangu ya simu na anwani yangu ya barua pepe ya hapo chini, naomba nishauri jambo moja kwa wasanii wetu hasa wanamuziki.

Unapoajiri mwanamuziki au unapoajiriwa kama mwanamuziki wa kundi fulani, unapomshirikisha mwenzako kwenye wimbo wako au unaposhirikishwa katika wimbo wa msanii mwingine, hakikisha yanakuwapo makubaliano ya maandishi kuhusu mahusiano yenu kiutendaji yanayojumuisha uhalali wa umiliki wa kazi mlizofanya, mipaka ya matumizi ya kazi hizo kibiashara na matumizi mengine na yote mtakayoona yanafaa.

Nashauri hivi kwa sababu nyimbo sasa ni mali, ni bidhaa ya thamani kama bidhaa nyingine. Tofauti na zamani watu wapolikuwa wakigombea nyimbo kwa ufahari tu, sasa watu wanazigombania kimaslahi.

Makubaliano hayo yatatofautiana baina ya washirika tofauti, watu tofauti na vikundi tofauti. Lazima yawe ya hiari, yanayofikiwa kwa moyo safi.

Maana yangu ni kwamba isiwepo “drafti” moja ya makubaliano inayonakiliwa tu kwa kubadili majina na tarehe bali kila makubaliano lazima yawe mapya na ya vipengee vinavyohusika na jinsi pande mbili zinavyokubaliana.

Hii ni muhimu sana kufanyika kwani itaepusha migogoro miongoni mwa wasanii wetu na hivyo kuepusha uhasama miongoni mwao unaoathiri maendeleo yao.

Wakati nikiwaomba wadau mnijibu swali langu, nawaomba Sikinde wasiuache wimbo wa “Hamnazo” kwenye albamu yao huku nikiwashauri wasanii wote kutunza vizuri kazi zao za sanaa wanazomiliki kihalali kama wanavyotunza mali nyingine ili nazo ziwemo kwenye orodha ya mali za mirathi siku zetu za kuwa duniani zitakapofikia tamati.

Je, wimbo ni mali ya nani miongoni mwa wanamuziki wa Tanzania? Nasubiri jibu.

 

Makala hii ilichapishwa kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 12 Aprili, 2012

Toa Maoni Hapa

Added by

daniel

SHARE

Your email address will not be published. Required fields are marked *